MWENYEKITI wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba akiongea katika mkutano na
wanahabari leo katika ofisi za Tume jijini Dar es Salaam. Kulia ni
Katibu wa Tume Bw. Assaa Rashid.
..........................................................
Na Omega S. Ngole,
Wananchi
wenye sifa za kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na ambao wangependa
kuwa Wajumbe wa Mabaraza wanaweza kuanza kuwasilisha maombi yao kwa Maofisa
Watendaji wa Vijiji au Mtaa kuanzia kesho (Ijumaa, tarehe 8 Machi, 2013) hadi
tarehe 20 Machi mwaka huu (2013).
Kwa Zanzibar, maombi hayo yawasilishwe kwa
Masheha.
Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba amesema jijini Dar es
Salaam leo (Alhamisi, Machi 7) kuwa ili kuhakikisha mchakato wa uundwaji na
uendeshaji wa Mabaraza ya Katiba unaendeshwa kwa ufanisi, Tume imeandaa
Mwongozo wa kusimamia mchakato huo na kuuchapisha katika magazeti mbalimbali na
kuwekwa katika tovuti ya Tume (www.katiba.go.tz) na ukurasa wa facebook
wa Tume (tumeyamabadilikoyakatiba).
Jaji Warioba ameongeza kuwa Tume yake pia imechapisha
vitabu vyenye mwongozo huu na kuvisambaza kwa Ofisi za Wakuu wa Wilaya na
Wakurugenzi wa Miji, Manispaa, Majiji na wadau wengine kwa Tanzania Bara ili
wawafikishie wananchi katika mitaa na vijiji.
Kwa Zanzibar, mwongozo
umesambazwa kwa Ofisi za Wakuu wa Wilaya, Baraza la Manispaa na Katibu wa
Halmashauri za Mji ili wawafikishie wananchi katika Shehia zao.
“Sifa za mwananchi anayependa kuomba nafasi ya kuwa
mjumbe wa Baraza la Katiba ni pamoja na kuwa raia wa Tanzania na awe na umri wa
miaka 18 au zaidi,” amesema Jaji Warioba katika mkutano wake na wanahabari uliofanyika
katika ofisi za Tume
Jaji Warioba alitaja sifa nyingine kuwa ni pamoja na
kuwa na uwezo wa kusoma na kuandika na pia awe ni mkazi wa kudumu wa Kijiji,
Mtaa au Shehia husika.
Sifa nyingine ni pamoja na kuwa mtu mwenye hekima,
busara na uadilifu na ambaye ana uwezo wa kujieleza na kupambanua mambo.
Katika mwongozo huo, Jaji Warioba amesema, Tume pia
imeelekeza kuwa wananchi wanaoomba wanapaswa kuwasilisha nakala mbili za barua
ya maombi.
Barua moja itabaki katika Ofisi ya Mtendaji na barua ya pili atabaki
nayo mwombaji baada ya kutiwa saini na kugongwa muhuri kuthibitisha kuwa ombi
lake limepokelewa.
Aidha, baada ya muda wa kuwasilisha maombi kukamilika, Tume
imeelekeza katika mwongozo wake kuwa majina ya waombaji wote yatapaswa kuwa
katika sehemu za wazi na mbao za matangazo za ofisi za Watendaji wa mitaa au
vijiji kuanzia tarehe 22 – 28 Machi mwaka huu ili wananchi waweze kuyapitia na
kujiridhisha kuwa maombi yao yamepokelewa.
Mwongozo wa Tume pia
umeelekeza kuwa kuanzia tarehe 30 Machi hadi 3 Aprili kutafanyika Mikutano
Mikuu Maalum ya Mitaa, Vijiji au Shehia kwa Zanzibar ili kufanya uchaguzi na
kufuatiwa na Vikao
Maalum ya Maendeleo vya Kata vitakayofanyika kati ya tarehe
5 hadi 9 Aprili mwaka huu ili kuchagua wawakilishi wa kila wa Kata. Majina hayo
yatawasilishwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji, Manispaa au Jiji kwa
Tanzania Bara na Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa, Katibu wa Halmashauri Mji/
Wilaya kwa Zanzibar ambao watayawasilisha kwa Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba kwa uteuzi rasmi.
Jaji Warioba
amewaomba wananchi na viongozi wote kuendesha mikutano ya uundwaji wa mabaraza
kwa amani na utulivu na kuzingatia mwongozo uliotolewa na Tume.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment